Thursday, March 24, 2016

Maji ya mvua ni salama kwa kunywa?

Katika maeneo yenye uhaba wa maji ya bomba, mvua ni chanzo muhimu sana cha maji ya kunywa katika ngazi ya kaya. Hivi karibuni msomaji wetu mmoja aliuliza; “Je, kuna tatizo lolote wanapata watu wanaotumia maji ya mvua kwa ajili ya kunywa?”

Kwa asili yake maji ya mvua kabla hayajafika katika anga letu huwa ni safi na salama kwa kunywa. Hata hivyo, maji hayo lazima yapite katika anga na ndipo yafike ardhini kama mvua.

Hapo ndipo hatari ya maji ya mvua inapoanza na kuongezeka zaidi yanapofika katika paa la nyumba au sehemu maalumu iliyojengwa kuvuna maji hayo na hatimaye kuhifadhiwa katika ndoo au tenki.

Maji ya mvua yanapopita katika anga hubeba vumbi, moshi na gesi mbalimbali zikiwamo carbon dioxide, oxygen, nitrogen dioxide na sulfur dioxide. Vitu hivyo hupunguza usafi na usalama wa maji ya mvua.

Uchafuzi zaidi wa maji ya mvua hutokea pale yanapofika katika paa la nyumba au sehemu maalumu iliyojengwa kuyavuna.

Maji ya mvua yanapofika katika paa au sehemu inayotumika kuyakusanya mara nyingi hubeba kemikali, vumbi, mchanga, vitu vilivyooza, majani, vinyesi vya ndege na wanyama.

Maji kama hayo yanapoingia katika chombo cha kuhifadhia yanaweza kuwa mazalia mazuri ya vijidudu vinavyosababisha magonjwa ya tumbo kama vile kuhara, homa ya tumbo, kipindupindu na hata kuzalisha mbu wanaoeneza magonjwa mbalimbali mfano malaria.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa maji ya mvua mara tu baada ya kuvunwa huwa na vijidudu vinavyosababisha magonjwa ya tumbo, vikiwamo Giardia, Cryptosporidium, E. coli, Campylobacter, Vibrio, Salmonella, Shigella na Pseudomonas.

Maji ya mvua lazima yachemshwe kabla ya kuyatumia kwa kunywa au kupiga mswaki.

Idadi kubwa ya uchafu na vijidudu hupatikana pale mvua inapoanza kunyesha.

Watu wanashauriwa waanze kukinga au kuvuna maji dakika tano baada ya mvua kuanza kunyesha ili paa la nyumba au sehemu ingine inayotumika kukusanya maji ijisafishe kwa mvua ya kwanza.

Kwa kawaida, maji ya mvua hayana kiwango hatari cha kemikali zinazodhuru afya. Hata hivyo, mara nyingine kiwango cha kemikali ya zinc na lead huwa kikubwa kutokana na kuingia kemikali hizo kutoka katika paa la nyumba, tenki la kuhifadhia maji au angani.

Watu wanaovuna maji ya mvua kwa kiasi kikubwa, wanahimizwa kupima maji yao katika maabara za maji pale wanapoyavuna na miezi kadhaa baada ya kuyahifadhi.

Maji ya mvua yana uchachu na kiwango kidogo cha madini. Kiwango kidogo cha madini katika maji ya mvua kinayafanya maji hayo kukosa ladha ukilinganisha na maji ya kisima, mto, ziwa au bomba.

Kiasi kidogo cha madini kama calcium, magnesium, iron, na fluoride ni muhimu katika maji ili kuimarisha afya. Katika baadhi ya nchi, maji ya mvua husafishwa na kuongezwa madini muhimu kiafya na kusambazwa kwa wananchi kama maji ya kunywa.

Usafi na usalama wa maji ya mvua unategemea usafi wa paa la nyumba, gata, bomba na ndoo au tenki la kuhifadhia maji.

Wiki ijayo nitaelimisha juu ya namna bora na sahihi ya kuhifadhi maji ya mvua hasa katika matenki. Hii itasaidia sana jamii ya watu wa kipato cha chini ambao hutumia gharama kubwa kwa ajili ya kununua na kutumia muda mrefu wakitafuta maji.

No comments:

Post a Comment