Thursday, March 17, 2016

BILIONI 18.77 KUTUMIKA KWENYE ELIMU BURE INCHI NZIMA.

SERIKALI imeshatoa Sh bilioni 18.77 hadi sasa katika kufanikisha mpango wa elimu bure. Aidha, imesema itaendelea kujipanga kuhakikisha inaendelea kuwaondolea mzigo wa gharama za elimu Watanzania huku ikisisitiza watoto wapelekwe shule.

Kuanzia Januari mwaka huu, Serikali ya Awamu ya Tano imefuta ada na michango isiyo na tija iliyokuwa ikitozwa kwa wanafunzi kote nchini, hali iliyoibua ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule nchini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyasema hayo juzi mjini hapa wakati akizungumza na watumishi wa umma na viongozi wa Mkoa wa Kagera katika siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani humo.

Alisema serikali imetangaza Sh bilioni 131.6 kwa ajili ya kufanikisha elimu bure nchini kwa miezi sita na hadi sasa imekwisha toa Sh bilioni 18.77 zilizopelekwakatika shule mbalimbali za msingi na sekondari.

“Lakini kumekuwapo na changamoto mbalimbali katika utoaji wa elimu bure nchini. Lipo suala la madawati, nyumba za walimu, upungufu wa walimu. Zote hizo zinafanyiwa kazi,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

“Serikali itaendelea kujipanga kuzidi kupunguza mzigo wa kugharamia elimu kwa mwananchi,” aliongeza. Alisema serikali inataka kuona watoto wote wanakwenda shuleni na kuagiza wenye umri wa miaka minne na mitano waandikishwe madarasa ya awali, kwani hakuna atakayeanza la kwanza bila ya kupita darasa la awali.

Alieleza kuwa watendaji wa vijiji kuhakikisha watoto hao wanaandikishwa katika madarasa ya awali na kwamba hilo sio jukumu la walimu, bali walimu jukumu lao ni kushughulikia taaluma.

“Watendaji wa vijiji ndio wanaojua baba wa watoto hao, hivyo ndio wenye jukumu la kuwasaka watoto hao mitaani, sio jukumu la walimu,” alifafanua Majaliwa na kuagiza Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanafunzi 79 ambao hawajaripoti kidato cha kwanza, kufanya hivyo ifikapo Machi 30, mwaka huu.

Aidha, alisisitiza kuwa suala la madawati limeachwa mikononi mwa wakuu wa mikoa na wilaya, hivyo hadi kufikia Juni mwaka huu, wawe wamekamilisha kazi hiyo. Pia alisisitiza kuhusu elimu kwa mtoto wa kike na kuwaagiza watendaji wa vijiji kupiga marufuku ngoma za usiku au madisko yenye ushawishi kwa wasichana.
Share: Facebook Twitter Google+

No comments:

Post a Comment